Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusufu Mwenda, ameahidi kushirikiana Kwa karibu na wafanyabiashara, kuhakikisha kuwa wanapata msaada unaohohitajika ili kufanikisha malengo ya Serikali Katika kukuza uchumi wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa.
Mwenda amebainisha hayo katika kikao cha wafanyabiashara kilichofanyika katika Manispaa ya Iringa ambapo amesema mamlaka itaendelea kuboresha mazingira yanayowezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati, ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Katika mkutano huo, Mwenda alielezea hatua mbalimbali zitakazochukuliwa kuboresha huduma za TRA, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya teknolojia na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Mwenda amesisitiza kuwa kulipa kodi si tu ni wajibu, bali pia ni fursa ya kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Vilevile Yusuph Mwenda amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo Mkoani Iringa kwa uadilifu wao na kutokuomba rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wakati wanatimiza majukumu yao.
“Watumishi wa TRA ni waadilifu, huwa hawaombi rushwa, kama ikitokea umeombwa rushwa toa taarifa kwenye vyombo husika na unaweza kuniambia mimi moja kwa moja”, amesema Mwenda.
Hapo awali baadhi ya wafanyabiashara waliwasifia na kuwapongeza Maafisa wa TRA kuwa ni watu wazuri na rafiki katika kutimiza majukumu yao.
Sambamba na hayo, Mwenda amewahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi ili nchi iendelee kujengwa huku akiahidi kuendelea kusimamia uwezeshaji wa biashara zao.