Gwiji wa tenisi Rafael Nadal ametangaza azma yake ya kustaafu hivi karibuni kutoka kwenye mchezo huo baada ya kazi yake nzuri ambapo alinyakua mataji 22 makubwa ya slam.
Anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa tenisi wa wakati wote, mchuano wa mwisho wa Nadal utakuwa na Uhispania kwenye fainali za Kombe la Davis mnamo Novemba.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alicheza mara ya mwisho kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris lakini kuendelea kukabiliwa na majeraha, ambayo yamemtatiza katika maisha yake yote mchezoni, yamepunguza sana muda wake wa kukaa uwanjani katika misimu miwili iliyopita.
“Halo watu wote, niko hapa kuwajulisha kuwa ninastaafu kutoka kwenye tenisi ya kulipwa,” Nadal alisema kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii.
“Ukweli ni kwamba imekuwa miaka ngumu, hii miwili iliyopita haswa. Sidhani kama nimeweza kucheza bila mapungufu.
“Ni wazi ni uamuzi mgumu, ambao umenichukua muda kufanya. Lakini katika maisha haya, kila kitu kina mwanzo na mwisho.