Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa hatakabiliwa tena na mashtaka ya uhalifu kuhusu kashfa ya fedha ambayo ilifichuliwa zaidi ya miaka miwili iliyopita nyumbani kwake na kusababisha uchunguzi wa kitengo maalum cha polisi, waendesha mashtaka walisema Alhamisi.
Mkuu wa zamani wa usalama wa taifa aliwasilisha malalamiko ya jinai dhidi ya Ramaphosa mnamo Juni 2022, akimtuhumu kwa utekaji nyara, hongo na uhalifu mwingine kuhusiana na wizi wa dola 580,000 za noti za Marekani ambazo zilifichwa kwenye kochi kwenye ranchi ya rais.
Bosi huyo wa zamani wa usalama, Arthur Fraser, alidai kuwa Ramaphosa alikuwa akihifadhi fedha hizo kwenye samani kwenye ranchi yake ili kukwepa sheria za fedha za kigeni za Afrika Kusini zilipoibwa.
Alinusurika katika kashfa hiyo na alichaguliwa tena kama kiongozi wa Afrika Kusini mwezi huu wa Juni, huku uchunguzi wa uhalifu ukiendelea. Ramaphosa, 71, pia alishtakiwa kwa utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na kukiuka sheria za fedha za kigeni kuhusu fedha hizo.
Alikanusha kufanya makosa na kusema fedha hizo zilitokana na mauzo halali ya nyati katika shamba lake la Phala Phala.