Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekagua ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi) lenye urefu wa kilometa 3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66, linalojengwa kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita kupita Ziwa Victoria ambao umefikia asilimia 93, leo Oktoba 13, 2024 Mkoani Mwanza
Ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa shilingi Bilioni 716.3 zikijumuisha Malipo ya Mkandarasi, Mhandisi Mshauri wa usimamizi wa mradi, Fidia na Usanifu.
Akitoa taarifa ya mradi, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa wakati ili ujenzi wa daraja hilo uweze kukamilika na kutumika ifikapo mwezi Februari, 2025.
Bashungwa ameeleza kuwa Mkandarasi amekamilisha kumwaga zege kwenye daraja lote na anaendelea na ujenzi wa barabara za maungio kilometa 1.66 kwa kiwango cha lami pamoja na kuweka mazingira ya daraja safi kwa kujenga kingo na kuweka alama za usalama.
Mradi wa ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli unasimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) chini ya Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation akishirikiana na China Railway 15 Bureau Group Corporation (CCECC – CR15G JV) na kusimamiwa na Mhandisi Mshauri kampuni ya Yooshin Engineering Corporation (Korea) akishirikiana na Cheil Engineering Co. Ltd (Korea), Rina Consulting S.P.A (Italia) na Afrisa Consulting Ltd (Tanzania).