Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imeahidi kutekeleza sheria mpya inayopiga marufuku vyombo vya habari kuchapisha picha za viumbe hai na Wizara ya Maadili ya Taliban, kupitia Msemaji wake Saiful Islam Khyber, imetangaza kuwa utekelezaji wa sheria hiyo utafanyika hatua kwa hatua huku wakiwataka Watu kukubaliana na tafsiri yao ya sheria za Kiislamu, Khyber amesema lengo ni kuwashawishi Watu kuwa Picha za Viumbe hai zinapingana na sheria za Kiislamu na utekelezaji wa sheria hiyo hautalazimishwa bali utafuata mbinu za ushauri na kufafanua umuhimu wake.
Inaelezwa kuwa Sheria hii mpya imeweka masharti mengine kadhaa kwa vyombo vya habari ikiwemo kuepuka kuchapisha Picha za Viumbe hai na kutokudharau au kupinga mafundisho ya Dini ya Kiislamu, hata hivyo sheria hii haijaanza kutekelezwa kwa ukali katika maeneo yote ya Nchi ikielezwa kuwa kwa sasa uchapishaji wa Picha kwenye mitandao ya kijamii bado unaendelea, ingawa juhudi za kutekeleza sheria hiyo zimeanza katika baadhi ya maeneo kama Kandahar, Helmand, na Takhar.
Aidha Waandishi wa habari kutoka Mikoa mbalimbali wamepokea taarifa kuhusu utekelezaji wa sheria hii kwa taratibu na Mkoani Ghazni, maafisa wa maadili wa Taliban waliwaita waandishi wa habari na kuwaelekeza kupunguza uchukuaji wa Picha na kuepuka matukio mengi ili kuanza kujifunza taratibu hiyo mpya, hali kama hiyo pia imetokea katika Mkoa wa Maidan Wardak ambapo Waandishi wa habari walijulishwa kuwa sheria hiyo itaanza kutekelezwa kwa hatua.
Afghanistan imeendelea kuporomoka katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari ambapo idadi ya Wafanyakazi wa vyombo vya habari imepungua kutoka 8,400 mwaka 2021 hadi 5,100, huku Wanawake wakiwa ni 560 tu, kwa mujibu wa Ripoti ya Waandishi Wasio na Mipaka (RSF), Afghanistan sasa inashika nafasi ya 178 kati ya nchi 180 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari.