Inasemekana kuwa klabu ya Barcelona tayari wametanguliza “uboreshaji wa mkataba wa kimkakati” wa Pedri, Gavi na Ronaldo Araujo, ambaye mikataba yake yote inamalizika 2026, kulingana na Mundo Deportivo.
Huku dirisha la uhamisho likiwa limefungwa, Barca wanataka kuhakikisha vipaji vyao vya vijana kwa mikataba ya muda mrefu iwezekanavyo ili kuepuka sakata zozote.
Kuna matumaini kwa Pedri na Gavi, huku ripoti ikidai kuwa viungo hao wawili wana uwezekano wa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Catalan kabla ya msimu kuisha.
Hata hivyo, bado kuna sintofahamu kuhusu mustakabali wa beki wa Uruguay, Araujo, ambaye ni majeruhi na hatarajiwi kurejea hadi mwisho wa mwaka.
Barca haijapokea jibu kutoka kwa mawakala wake kuhusu ofa waliyotoa zaidi ya mwezi mmoja uliopita, lakini klabu bado inamtaka aongeze mkataba wake kwa sababu inamchukulia kama sehemu muhimu ya mradi wa kocha mpya Hansi Flick.
Bayern Munich, pamoja na vilabu vingi vya Uingereza, hapo awali wameonyesha nia ya kutaka kumnunua Araujo, ambaye Barca wanatumai kuwa watawasiliana na maajenti wake kwamba nia yake ni kubaki kwenye kikosi cha LaLiga.
Mazungumzo yataongozwa na mkurugenzi wa michezo Deco na rais Joan Laporta, huku Barca wakiwa tayari kuwapa wachezaji wote watatu kandarasi hadi 2030.