Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu katika taarifa yake imesema itaangazia ushauri wa Marekani lakini itajibu shambulio la kombora la Iran kulingana na masilahi ya taifa lake.
Rais wa Marekani Joe Biden ameionya Israeli dhidi ya kushambulia vinuu vya nyukilia vya Iran au hata vituo vyake vya mafuta kama njia moja ya kuzuia kuongezeka kwa mzozo katika eneo la mashariki ya kati.
Wataalam wa masuala ya kuichumi wameonya kwamba wasiwasi iliopo kati ya Iran na Israeli huenda ikichangia kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani iwapo Israeli itashambulia vituo vya mafuta ya Iran.
“Tunasikiliza mapendekezo ya Marekani ila tutafanya uamuzi wetu wa mwisho wenyewe kwa mujibu wa masilahi ya taifa letu,” imesema ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli.
Taarifa hiyo imekuja baada ya ripoti ya jarida la The Washington Post la nchini Marekani, ilioeleza kwamba Netanyahu alikuwa ameihakikishia White House kwamba mashambulio yoyote ya kulipiza kisasi yatalenga tu maeneo ya kijeshi peke.
Ripoti ya The Wall Street Journal, nayo pia ikiwanuku maofisa kutoka nchini Marekani ilisema kwamba hakikisho hilo liliafikiwa kwa njia ya simu wiki iliopita kati ya Netanyahu na Biden.
Aidha inaripotiwa kwamba hakikisho hilo la Israeli pia liliafikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa Israeli, Yoav Gallant.