Waziri wa afya wa Rwanda Dkt. Sabin Nsanzimana amesema idadi ya watu wanaokufa kutokana na virusi vya Marburg nchini Rwanda imekuwa chini kuliko idadi ya watu wanaopona, na kuonesha kuwa juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo zikionyesha matokeo chanya.
Akiongea na wanahabari kuhusu hali ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo, Dkt Nsanzimana amesema jumla ya watu 61 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya Marburg, 14 wamefariki na wengine 27 wanaendelea na matibabu, idadi ya jumla ya watu waliopona imefikia 20, na hakuna mgonjwa mpya aliyerekodiwa.
Amesema kuna matumaini ya kuwa na uwezo wa kudhibiti virusi hivyo, ambavyo vimewaathiri zaidi wahudumu wa afya, baada ya kuonekana kuwa idadi ya watu wanaopona ni kubwa kuliko ya wanaokufa, ambayo ni ishara nzuri kwamba juhudi zilizopo zina matokeo chanya.