Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kufikia Oktoba 19, 2024, Jumla ya watanzania wenye sifa Milioni 26, 769,995 sawa na asilimia 81% wamejiandikisha kwenye daftari la Mpigakura, tayari kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Waziri Mchengerwa ametoa takwimu hizo leo Jumapili Oktoba 20, 2024 akiwa Wilayani Rufiji Mkoani Pwani, akiitaja Mikoa ya Tanga, Pwani, Mwanza, Dar Es salaam na Dodoma kuwa Vinara katika uandikishaji huo.
Mhe. Mchengerwa kando ya Kutangaza kutoongezwa kwa siku za kujiandikisha, amewashukuru watanzania wote waliotumia haki yao Kikatiba katika kujiandikisha kwenye Daftari hilo, akiwataka pia wale wote wenye sifa za kuwania nafasi mbalimbali za Uongozi kujitokeza kwa wingi kuanzia Oktoba 26, 2024 ili kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali kwenye serikali za Mitaa.
Mhe. Mchengerwa kadhalika ametoa wito kwa wasimamizi wa Uchaguzi na wadau wote wa Uchaguzi kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia Uchaguzi huo, akihimiza pia suala la usimamizi na utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha haki, usawa na Uhuru wa kuchagua unatamalaki kwenye Uchaguzi huo wa baadae mwaka huu.