Jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana ili kupunguza changamoto za watoto wenye uhitaji pamoja na watu wengine wanaoishi kwenye mazingira magumu na kujenga jamii yenye umoja na mshkamano bila kujali changamoto ambazo binadamu tumekuwa tukizipitia.
Wito huu umetolewa na Gerlad Masanya ambaye ni kiongozi wa timu ya LBL G SEAL walipofika katika shule ya msingi Ilembula ili kuwaona watoto wenye uhitaji pamoja na kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi wenye uhitaji katika shule hiyo.
“Tunajua tulichotoa sio kingi lakini kitawasaidia,lengo kubwa la kuja hapa ni kuendelea kuhamasisha jamii kwa kuwa serikali inafanya mengi lakini peke yake haitoweza hivyo jamii nzima tukishikana tunauhakika wa kupunguza uhaba wa vitu vinavyohitajika”amesema Masanya
Fred Mpogolo ni miongoni mwa walimu katika shule hiyo anayeshughulika na watoto wenye shida ya uoni ambapo amesema licha changamoto mbalimbali ambazo shule imekuwa ikikabiliwa nazo kwa wanafunzi wenye changamoto mbalimbali lakini serikali imekuwa mstali wa mbele kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki ya kupata elimu huku wakiomba wadau kusaidia vifaa vya kasasa kwa ajili ya maadalizi ikiwemo ya mitihani.
“Tuna vifaa ambavyotunavitumia lakini ni analog tungepata wadau wa kutusaidia vifaa vya kisasa vingeweza kutusaidia katika kuandaa vizuri zaidi mitihani kwa ajili ya wanafunzi wasioona”amesema Mwalimu Mpogolo.
Nao baadhi ya wanafunzi akiwemo Ashery Mwaisubile,Aripina Sanga pamoja na Frolence Mahenge kwa niaba ya wanafunzi wengine wameshukuru kwa msaada waliopata kwa madai kuwa umekwenda kupunguza changamoto za baadhi mahitaji ambayo wamekuwa wakihitaji.
Mahitaji mbali mbali ikiwemo Sukari,Chumvi,Sabuni,Majaba,dishi,madaftari,kalamu pamoja na leso vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Milioni moja na laki nane,vimekabidhiwa kwa wahitaji katika shule hiyo.