Hezbollah mapema Jumanne asubuhi ilisema ilirusha makombora katika vituo viwili muhimu karibu na Tel Aviv na kituo cha jeshi la wanamaji magharibi mwa Haifa, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akitarajiwa kuwasili Israel kuzindua msukumo mwingine wa kusitisha mapigano.
Juhudi za kidiplomasia hadi sasa zimeshindwa kumaliza vita vya Gaza vilivyodumu kwa mwaka mzima na mzozo kati ya kundi la waasi la Lebanon Hezbollah na Israel, ambao umeshika kasi katika wiki za hivi karibuni baada ya mwaka mmoja wa kurushiana risasi katika mpaka wa kusini mwa Lebanon.
Baada ya usiku mzito wa mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon na vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wake, Hezbollah ilisema kuwa imerusha makombora kwenye kituo cha Glilot kinachotumiwa na kitengo cha 8200 cha ujasusi wa kijeshi wa Israel, na eneo la Nirit katika vitongoji vya Tel Aviv.
Kundi hilo lilisema pia lilirusha makombora katika kambi ya wanamaji nje ya mji wa bandari wa Haifa kaskazini zaidi.
Hakukuwa na ripoti za mara moja za majeruhi. Mamlaka ya Israel ilisema ving’ora vya anga viliwashwa katika maeneo ya kusini mashariki mwa Tel Aviv kutokana na kombora moja lililotambuliwa kuvuka kutoka Lebanon na kuanguka katika eneo la wazi. Ving’ora vingine vilisikika huko Tel Aviv.
Vikosi vya ulinzi wa anga vya tabaka nyingi vya Israel vimenasa idadi kubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa dhidi yake tangu kuanza kwa vita vya Gaza.