Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ameagiza Mamlaka za udhibiti na usimamizi wa biashara nchini kuachana na dhana ya kukimbilia kufunga na kukwamisha wajasiriamali wadogo ambao hawajatimiza vigezo vya kisheria badala yake wawe walezi kwa kuwaelekeza hatua za kufuata ili wawe walipa kodi wakubwa.
Kigahe ametoa Maelekezo hayo mapema leo wakati akifungua maonesho ya tatu ya Biashara ya ‘Tanzanite Manyara Trade Fair 2024’ Mjini Babati, Manyara yanayohudhuriwa na wajasiriamali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Niziagize Mamlaka zinazosimamia na kudhibiti biashara kuwalea na kuwapa miongozo sahihi wajasiliamali badala ya kuwafungia pindi wanapokosea ili kuendeleza kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema Naibu Waziri Kigahe.
Kwa Upande wake Meneja Biashara Mati SuperBrand Gwandumi Mpoma ambao ni wadhamini wakuu, amewaomba wajasiliamali kuendelea kujitokeza kushiriki maonesho hayo ili kuweza kutangaza bidhaa zao zaidi.
Ametoa rai kwa Makampuni mengine makubwa kujitokeza kudhamini maonesho hayo ili kuisaidia serikali ili kuwasaidia wajasiliamali na wafanyabiashara ambapo huu ni mwaka wa tatu mfululizo tokea waanze kudhamini.
Ameongeza kuwa mwamko wa wafanyabishara wa mkoa wa Babati wamekosa mwamko wa kushiriki na kuzidiwa na wageni ambao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kutoka nchi mbali mbali kama vile Uganda, Kenya.
Nae Katibu mtendaji Chama cha Wafanyabiashara- TCCIA mkoa wa Manyara Zainabu Rajabu amesema maonesho ya mwaka huu yamehudhuriwa na washiriki 337 chini ya kauli mbiu ya “Manyara kwa ustawi wa biashara na uwekezaji” huku baadhi ya wajasiriamali walioshiriki wakifurahia kukutanishwa na wateja ma marafiki wa kibiashara.
Maonesho ya tatu ya Biashara ya Tanzanite Manyara trade fair 2024 yaliyoanza Oktoba 20 yataendelea hadi Oktoba 30.