Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi ametangaza mipango ya kuunda tume ya kuchunguza marekebisho ya katiba ya nchi hiyo, uwezekano wa kuondoa ukomo wa mihula na kuandaa njia ya kuwania muhula wa tatu.
Uamuzi wa Tshisekedi wa kushughulikia masuala yenye utata ya mageuzi ya katiba na muhula wa urais unaweka hatari ya kulisukuma taifa hilo lenye utajiri wa madini, ambalo limevumilia miongo kadhaa ya migogoro, kuingia katika mzozo zaidi wa kisiasa na machafuko.
Tshisekedi aliapishwa kushika wadhifa huo mwezi Januari baada ya uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Disemba kwa muhula wa pili na wa mwisho. Siku ya Jumatano aliweka mipango ya kuangalia marekebisho ya katiba, akisema katiba ya sasa, iliyoidhinishwa na kura ya maoni mwaka 2005, haiendani na hali halisi ya sasa ya nchi.
“Mmesikia kuhusu uwezekano wa mabadiliko ya katiba, hatupaswi kuogopa kuwa somo hili litashughulikiwa,” Tshisekedi aliwaambia wafuasi wake mjini Kisangani, akiongeza kuwa ana mpango wa kuunda tume kuanza kufanyia kazi suala hilo mwaka ujao.
“Hii hadithi ya mihula miwili ambayo Katiba ya sasa inaitaka, lazima wananchi waamue iwapo wanataka tubadilike,” alisema. Tshisekedi pia alipendekeza kuwa wale ambao hawakukubaliana na uamuzi wake walikuwa wakitumia suala hilo kugawanya taifa.