Tume ya Uchaguzi ya nchini Msumbiji imemtangaza Daniel Chapo kutoka chama cha Frelimo kama mshindi wa kiti cha Urais kufuatia Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Oktoba 9, 2024.
Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji, Chapo amepata asilimia 70 ya kura zote zilizopigwa, huku Venancio Mondlane kutoka chama cha Podemos akivuna asilimia 20 ya kura kwenye uchaguzi huo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa siku ya Oktoba 24, yanakifanya chama tawala cha Frelimo kuendeleza wake katika nchi hiyo inayopatikana kusini mwa Afrika, licha ya malalamiko ya wizi wa kura kutoka vyama pinzani nchini humo.
Chapo, mwenye umri wa miaka 47, anakuwa Rais wa tano wa Msumbiji, akichukua nafasi ya Filipe Nyusi, ambaye muhula wake wa vipindi viwili umefikia kikomo.
Kulingana na wasimamizi wa uchaguzi huo, mchakato huo haukuwa wa huru wala haki, huku Umoja wa Ulaya ukiainisha baadhi ya makosa wakati wa zoezi la kuhesabu kura.
Hata hivyo, tume hiyo imekana madai hayo.
Kwa upande wake, Mondlande ambaye amejitangazia ushindi, ameitisha maandamano ya nchi nzima siku ya Alhamisi na Ijumaa.