Waziri mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Urusi, Bw. Maxim Reshetnikov na kujadiliana naye masuala mbalimbali yakiwemo yanayogusa biashara, kilimo, usafirishaji, elimu, nishati na utalii.
Akizungumza na Waziri Reshetnikov leo (Jumatatu, Oktoba 28, 2024) ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amemhakikishia Waziri huyo kwamba Tanzania ni mahali pazuri pa kufanya biashara kwa kuwa ni nchi tulivu na Mwenyezi Mungu ameiweka mahali pa kimkakati pa kuweza kufanya biashara.
“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua kufanya maboresho kwenye biashara kati ya Tanzania na nchi marafiki, Urusi ikiwemo. Kupitia ziara hii, nina uhakika mtapata maelezo mazuri ambayo yatawatia moyo wa kuiamini Tanzania kwamba ni mahali pazuri pa kufanyia biashara,” amesema,
Akielezea kuhusu fursa zilizopo nchini, Waziri Mkuu amesema Tanzania inapakana na bahari yenye bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. “Ina maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa na yenye bandari kadhaa. Ziwa Victoria kuna bandari kule Kagera, Mwanza na Musoma. Ziwa Tanganyika kuna bandari za Kigoma, Kabwe na Kasanga na Ziwa Nyasa kuna bandari za Mbambabay na Kyela.”
Amesema bandari hizo zimeunganishwa na barabara, reli ya kati, TAZARA, reli ya SGR na vyote vinaenda hadi nje ya nchi ili kurahisihwa usafirishaji wa bidhaa. “Tunao usafiri wa uhakika kutoka Dar es Salaam hadi Kapiri-Mposhi, Zambia ambako bidhaa zinachukuliwa na kupelekwa nchi nyingine. Pia SGR itakapokamilika, itawezesha kufikisha mizigo hadi Rwanda, Uganda na Congo.”
Kuhusu kilimo, Waziri Mkuu amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Urusi waje kuwekeza kwenye kilimo kwa kuwa Tanzania ina eneo kubwa la ardhi na lenye rutuba kwa ajili ya shughuli za uzalishaji. “Malengo ya Tanzania ni kuona tunakuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula barani Afrika.”
Ametumia fursa hiyo kumweleza faida mbalimbali za kuwekeza Tanzania kubwa ikiwa ni uhakika wa wateja kwa bidhaa zao kwani yenyewe ina wakazi zaidi ya milioni 61, ukanda wa Afrika Mashariki una watu zaidi ya milioni 300 na pia nchi za SADC ambako Tanzania ni wanachama, una uhakika wa soko la watu zaidi ya milioni 300.
“Tanzania ni lango kwa nchi nane zinazotuzunguka na mbili ziko mbioni kujiunga. Nchi hizo ni Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. Kuna nchi mbili za Comoro na Sudan Kusini ambazo nazo zimeonesha nia na pia Somalia tunaendelea na mazungumzo.”
Mapema, akitoa maelezo ya ujio wake, Waziri Reshetnikov alisema nchi hizo mbili zimeshakubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kukuza biashara na uwekezaji na ndiyo maana kesho (Jumanne, Oktoba 29, 2024) watakuwa na kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kiserikali ya Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Tanzania na Urusi chenye nia ya kuimarisha uhusiano huo. (First Meeting of the Russia-Tanzania Joint Intergovernmental Commission on Trade and Economic Cooperation.)
Alisema kikao hicho ni matokeo ya makubaliano ya kuanzishwa kwa Tume hiyo ya pamoja ambayo yalisainiwa Desemba 29, 2022 ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi.
Kwa upande wa elimu, Waziri huyo alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Watanzania kunufaika na fursa za masomo nchini Urusi kutokana na bajeti ya Serikali. “Hivi sasa kuna nafasi 90 za wanafunzi wa Kitanzania kusomea vyuo vikuu vya Urusi kuanzia mwaka ujao. Tuko tayari kuongeza idadi hiyo endapo itabidi,” alisema Waziri Reshetnikov.