Jengo moja liliporomoka katika kitongoji cha mji mkuu wa Nigeria mwishoni mwa juma, na kuua takriban watu saba, polisi walisema.
Polisi wa Abuja walisema jengo hilo lililo katika eneo la Sabon-Lugbe mjini Abuja, tayari lilikuwa limebomolewa kwa kiasi, na muundo wake uliathiriwa zaidi na wanyang’anyi waliokuwa wakitafuta vyuma chakavu.
Msemaji wa polisi wa Abuja Josephine Adeh alisema watu watano waliokolewa kutoka kwenye vifusi siku ya Jumapili.
Kuporomoka kwa majengo kunazidi kuwa jambo la kawaida nchini Nigeria, huku zaidi ya matukio dazeni kama hayo yamerekodiwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mamlaka mara nyingi hulaumu majanga kwa kukosa utekelezaji wa kanuni za usalama wa majengo na matengenezo duni.
Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ilirekodi majengo 22 yakiporomoka kati ya Januari na Julai mwaka huu, kulingana na Baraza la Udhibiti wa Uhandisi nchini Nigeria.
Mnamo Julai, shule ya orofa mbili ilianguka kaskazini-kati mwa nchi, na kuua wanafunzi 22. Saints Academy, iliyoko katika jamii ya Busa Buji katika Jimbo la Plateau, ilianguka muda mfupi baada ya wanafunzi hao, ambao wengi wao walikuwa na umri wa miaka 15 au chini zaidi, kuwasili.