Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na utekelezaji wa miradi 77 ya ujenzi wa barabara na madaraja kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) yenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.6.
Aidha, Serikali kupitia TANROADS tayari imekamilisha kwa asilimia 100 miradi 25 ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 1,198 iliyogharimu Shilingi Trilioni 1.68 katika kipindi cha utawala wa Rais Dkt. Samia.
Haya yamebainishwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta wakati wa akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) kwa kiwango cha lami sehemu ya pili inayoanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala (km 60).
Eng. Besta ameeleza tangu Rais Samia aingie madarakani ameweka kipaumbele katika ujenzi wa barabara na madaraja ili kurahisisha usafiri na usafirshaji na kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi 77 ya ujenzi wa barabara na madaraja yenye thamani ya takribani Triloni 4.6.
“Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja inaendelea kwa kasi maeneo mbalimbali nchini na hakuna mradi uliokwama kwasababu Serikali ya Rais Samia imekuwa ikilipa wakandarasi kulingana na mikataba”, amesema Besta.
Besta ameongeza kuwa hadi sasa Shilingi Bilioni 101.1 zimelipwa kwa Makandarasi katika miradi 24 ya barabara inayoendelea kutekelezwa pamoja na miradi ya minne (4) ya ujenzi wa viwanja vya ndege nchini.
Kadhalika, Besta ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigogo Busisi) ambalo linagharimu Shilingi Bilioni 717 limefikia zaidi ya asilimia 94.
Amefafanua kuwa kutokana na mafanikio ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini imeifanya Tanzania kuwa nafasi ya 6 kati ya nchi 54 za Afrika kuwa na mtandao bora wa barabara ikipanda kutoka nafasi ya 16 iliyokuwapo katika mwaka 2022 kulingana na Takwimu za Statista.com.