Ufikiaji wa mitandao ya kijamii nchini Msumbiji umezuiwa kwa mara ya pili ndani ya wiki moja, kulingana na shirika la kimataifa la uangalizi wa mtandao wa NetBlocks, kufuatia wito wa migomo ya nchi nzima ya viongozi wa upinzani kutokana na uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata.
Mvutano umeongezeka nchini Msumbiji baada ya chama tawala cha Frelimo, ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 49, kushinda uchaguzi wa Oktoba 9-matokeo ambayo vyama vya upinzani na waangalizi wa uchaguzi wanadai yalikuwa na dosari.
NetBlocks, shirika lenye makao yake makuu London linalofuatilia kukatika kwa mtandao, lilithibitisha kuwa majukwaa ya mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na Facebook, Instagram, na WhatsApp, yaliwekewa vikwazo.
Haya yanajiri baada ya awali kuzimwa kwa mtandao Ijumaa iliyopita, siku moja baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa na kufuatia msako mkali dhidi ya maandamano.
NetBlocks ilielezea kukatika kwa umeme kwa Ijumaa iliyopita kama “tatizo la karibu kabisa la muunganisho wa mtandao wa simu,” na kuathiri uwezo wa wananchi wengi wa Msumbiji kupata taarifa.
Daniel Chapo wa Frelimo alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais mnamo Oktoba 24, kwa karibu 71% ya kura. Venancio Mondlane, kiongozi wa chama cha Podemos, alishika nafasi ya pili kwa 20%.
Kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo kulizua maandamano, huku wafuasi wa upinzani wakiingia mitaani. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeripoti kuwa takriban watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa katika makabiliano na vikosi vya usalama.
Polisi wameeleza kuwa watu 20 walijeruhiwa na watu wawili walifariki lakini hawakutoa maelezo zaidi.