Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Edu Gasper anatarajiwa kuondoka klabuni hapo, hatua inayotajwa kuwa pigo kubwa kwa kocha Mikel Arteta.
Edu, Raia wa Brazil na kiungo wa zamani wa Arsenal amekuwa mshirika muhimu wa Arteta akihusika katika usajili wa wachezaji nyota kama Martin Odegaard, Kai Havertz na Declan Rice huku akiongoza mafanikio ya klabu katika masuala ya usajili na kuleta wachezaji wengine wengi walioboresha kikosi.
Edu amesifiwa kama mmoja wa Wakurugenzi wa Michezo bora Duniani kwa mchango wake mkubwa katika kubadilisha mfumo wa usajili wa Arsenal ambapo itakumbukwa aliposimamia kuondolewa kwa wachezaji wenye changamoto, kama Pierre-Emerick Aubameyang, ambao walionekana kuwa vichocheo enzi ya matokeo duni, ingawa sababu za kuondoka kwake hazijawekwa wazi, inadaiwa kuwa ni uamuzi wake mwenyewe, na taarifa zaidi zinatarajiwa kutolewa ndani ya saa 24 zijazo.
Tangu kuteuliwa kwake mwaka 2019, Edu ameleta mabadiliko makubwa ya kiutamaduni katika Arsenal, akitilia mkazo maadili ya klabu na kuweka msingi thabiti wa mafanikio pia ameonekana mara kwa mara kwenye picha rasmi za Klabu na Wachezaji wapya, akielezea malengo mapya na kuimarisha matumaini ya Mashabiki.
Kuondoka kwake kutaacha pengo kubwa, na Mashabiki wa Arsenal sasa wanangoja kwa hamu maelezo rasmi kutoka kwa uongozi juu ya sababu za uamuzi huo, Arteta anatarajiwa kuzungumzia suala hilo kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Milan, ambapo atatoa maoni yake kuhusu athari za kuondoka kwa Edu na jinsi Arsenal itakavyokabiliana na pengo hilo.