Takriban watu 472,000 wamekimbia Lebanon kuelekea Syria tangu Septemba 23, kufuatia kuongezeka kwa mzozo kati ya Israel na Hezbollah, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Idadi hiyo inajumuisha wakimbizi 32,829 wa Lebanon na wakimbizi 216,369 wa Syria ambao walikuwa wamekwenda Lebanon miaka iliyopita wakati nchi yao ilipokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wasyria hawa sasa wanarejea nchini mwao kwani hali ya Lebanon imekuwa ya sintofahamu sana.
Wengi wa waliowasili Syria, walikuwa wamekimbia kutoka kusini mwa Lebanon, ambako majeshi ya Israel yanafanya mashambulizi makali kila siku.
Vita vya Israel dhidi ya Gaza, kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023, vimeenea hadi Mashariki ya Kati kwa upana huku Tel Aviv sasa ikishambulia Lebanon kwa kile inachosema ni kampeni ya kijeshi ya kung’oa Hezbollah.
Takriban watu 2,897 wameuawa hadi sasa nchini Lebanon na 13,402 wamejeruhiwa, kulingana na Wizara ya Afya ya Lebanon.