Israel imesema Jumatatu kuwa imesitisha mahusiano yake na Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi wa Palestina UNRWA.
Wakati huo huo jeshi la Israel limedai kuwa limemuuwa kamanda mmoja mkuu wa kundi la Hezbollah anayedaiwa kuhusika na mashambulizi ya makombora kusini mwa Lebanon.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imesema kuwa imeufahamisha Umoja wa Mataifa kuhusiana na kusitishwa kwa mahusiano yake na UNRWA katika mkataba uliotiwa saini mwaka 1967.
Hatua hiyo ya Israel inaonekana ni mwendelezo wa sheria iliyopitishwa mwezi uliopita iliyotaka kuzuia shirika hilo kutofanya kazi nchini Israel.
Israel inasema shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeingiliwa na wanamgambo wa Hamas, madai ambayo UNRWA yenyewe inayakanusha na kudai kuwa inachukua hatua kuhakikisha kwamba haiegemei upande wowote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa upande wake limesemahatua hiyo ya Israel itasababisha kusambaratika kwa kazi ya misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza unaokabiliwa na vita.