Maafisa wa Ukraine waliripoti uharibifu wa majengo ya makazi Alhamisi baada ya mashambulio ya usiku ya ndege zisizo na rubani za Urusi, huku rais wa Korea Kusini akisema hatazuia kupeleka silaha kwa vikosi vya Ukraine.
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alisema kwenye Telegram kwamba shambulio la Urusi liliharibu nyumba na majengo ya ghorofa katika wilaya tano katika mji mkuu wa Ukraine.
Serhii Popko, mkuu wa Utawala wa Kijeshi wa Jiji la Kyiv, alisema ulinzi wa anga wa Ukraine ulidungua zaidi ya dazeni tatu za ndege zisizo na rubani katika mkoa wa Kyiv, na kwamba watu wawili walijeruhiwa.
Katika eneo la Odesa kusini mwa Ukraine, Gavana Oleh Kiper alisema Alhamisi mabaki ya ndege zisizo na rubani zilizoanguka ziliharibu majengo kadhaa na kujeruhi mtu mmoja.
Serhiy Lysak, gavana wa eneo la Dnipropetrovsk, aliripoti kwenye Telegram kwamba mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi ziliharibu nyumba tano kwa usiku mmoja, lakini hazikusababisha majeraha yoyote.
Maafisa wa Korea Kusini na Marekani wamesema Korea Kaskazini ina zaidi ya wanajeshi 10,000 waliotumwa katika eneo la Kursk nchini Urusi.