Mshambulizi wa Galatasaray, Victor Osimhen amerejea kwenye kikosi cha Nigeria baada ya kukosa mechi ya mwezi uliopita ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Libya.
Mshambulizi huyo wa Super Eagles, ambaye sasa amepona kabisa jeraha lililomweka nje ya raundi ya mwisho ya mechi, ni sehemu ya kikosi cha wachezaji 23 kitakachomenyana na Benin na Rwanda katika raundi mbili za mwisho za kufuzu kwa dimba la 2025.
Super Eagles itamenyana na Duma wa Jamhuri ya Benin Uwanja wa Stade Felix-Houphouet-Boigny mnamo Novemba 14, kabla ya kusafiri nyumbani Uyo kwa mchezo wa mwisho wa kufuzu dhidi ya Amavubi ya Rwanda Uwanja wa Godswill Akpabio mnamo Novemba 18.
Katika kikosi hicho pia yumo mchezaji anayewania tuzo ya Ballon d’Or, Ademola Lookman, ambaye pia anapendekezwa kurithi mikoba ya Osimhen kutwaa tuzo ya CAF ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wanaume.
Wakati kurejea kwa Osimhen ni habari njema, furaha itapungua kwa kukosekana kwa beki Semi Ajayi, ambaye amekuwa nje kwa miezi minne baada ya kusumbuliwa na kile kinachodaiwa kuwa ni kupasuka kwa misuli ya daraja la juu na kulazimika kufanyiwa upasuaji, kwa mujibu wa meneja wa West Bromwich Albion Carlos. Corberan.