Raia wa Burundi, Ferdnand Ndikuriyo(27) maarufu kama Chuma cha Chuma amegonga mwamba kuhusu dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na Hakimu anayesikiliza kesi yake kuanza likizo.
Chuma cha Chuma alifikishwa mahakamani hapo juzi, akikabiliwa na kosa la kuwepo nchini Tanzania bila kibali ambapo alikosa dhamana baada ya kuwekewa pingamizi ambalo leo Novemba 6, 2024 ilitakiwa litolewe uamuzi.
Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo ambapo iliitishwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.
Wakili wa Serikali, Grace Nyarata akisaidiana na Ezekiel Kibona alidai shauri hilo linasikilizwa mbele ya hakimu Swalo lakini ameanza likizo hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea.
Baada ya Grace kudai hayo mshitakiwa aliiomba mahakama itoe uamuzi ili aweze kupata dhamana kwa sababu ana mtoto mdogo nyumbani anaumwa na yeye ndo anategemewa kama msaada, hivyo aliomba apate dhamana ili akatoe msaada.
Wakili Kibona alidai kuwa waliwasilisha maombi yao na wameyaweka kwenye mfumo kuhusu pingamizi lao la mshitakiwa kutopata dhamana na kilichobaki ni kuwa wanasubiri kujua imepangwa kwa nani ili waweze kuendelea.
Hakimu alisema kwakuwa shauri halisikilizwi mbele yake hivyo hatoweza kutoa uamuzi wowote juu ya dhamana ya shauri hilo na kuwataka kuwasilisha maombi yao kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi ili aone kesi itapangwa kwa nani aweze kuendelea.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 19, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ilidaiwa Septemba 18, mwaka huu eneo la Upanga Las Vegas Casino wilaya ya Ilala Dar es Salaam mshitakiwa alibainika kuwepo nchini bila kibali.