Wanajeshi na polisi walishika doria katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, mapema Alhamisi kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyokataliwa na upinzani.
Ghasia zimelikumba taifa hilo la kusini mwa Afrika tangu chama cha Frelimo, ambacho kimetawala kwa takriban miaka 50, kiliposhinda uchaguzi wa Oktoba 9.
Jiji la zaidi ya watu milioni moja lilikuwa katika hali tete siku ya Alhamisi asubuhi, ambapo maduka, benki, shule na vyuo vikuu vilifungwa. Maelfu ya waandamanaji walikusanyika kwenye moja ya barabara kuu kabla ya kuamrishwa na askari kurudi nyumbani.
Daniel Chapo wa Frelimo alishinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 71 ya kura, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, huku mgombea mkuu wa upinzani Venancio Mondlane akiibuka wa pili kwa asilimia 20.
Mondlane, akiungwa mkono na chama cha Podemos na ambaye alisema matokeo yalikuwa ya uongo na kwamba yeye ndiye aliyeshinda, aliitisha maandamano makubwa siku ya Alhamisi.
Kwa kutumia mitandao ya kijamii, amewakusanya wafuasi wake barabarani tangu uchaguzi katika maandamano ambayo yamezua vurugu kutokana na ukandamizaji wa polisi.
Katika mahojiano na shirika la Habari la AFP, kiongozi huyo wa upinzani ambaye hajulikani aliko, alisema hatakuwepo kwenye maandamano hayo kutokana na wasiwasi wa usalama wake.