Sudan imeanza kutekeleza mpango wake wa kwanza wa chanjo ya malaria huku kukiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 18 nchini humo.
Chanjo zitatolewa kwa takriban watoto 148,000 walio chini ya umri wa miezi 12 katika maeneo 15 katika majimbo ya Gedaref na Blue Nile.
Sudan ni miongoni mwa nchi 16 za kwanza za Afrika kuanzisha chanjo ya malaria.
Kampeni hiyo inafanywa na Wizara ya Afya ya Shirikisho, kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Gavi, Muungano wa Chanjo.
Uzinduzi huo unafuatia kuwasili kwa shehena ya kwanza ya dozi 186,000 za chanjo ya malaria hadi Sudan mwezi Oktoba.
Chanjo hiyo inatarajiwa kuanzishwa katika tovuti 129 kote nchini mnamo 2025 na 2026.
Malaria huua karibu watoto nusu milioni walio chini ya umri wa miaka 5 kila mwaka barani Afrika kulingana na UNICEF.
Mnamo mwaka wa 2023, zaidi ya visa milioni 3.4 vya malaria vilikadiriwa nchini Sudan, na kusababisha vifo vinavyokadiriwa kufikia 7,900, ingawa UNICEF inaonya kuwa takwimu zinaweza kuripotiwa chini ya hali ya migogoro na kukatika kwa mawasiliano inayoendelea nchini humo.
Imependekezwa kwa watoto wenye umri wa miezi mitano hadi 12, chanjo hiyo inatarajiwa kupunguza kulazwa hospitalini kwa watoto na vifo kutokana na ugonjwa huo.
Vita nchini Sudan vimewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 14, au takriban 30% ya watu wote, tangu vilipozuka zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Umoja wa Mataifa unasema.