Bunge la Ghana jana Alhamisi liliahirishwa tena kwa muda usiojulikana kufuatia pingamizi la wabunge kutoka chama tawala cha New Patriotic Party (NPP) muda mfupi kabla ya uchaguzi.
Kukosekana wabunge wa chama tawala cha NPP kulisimamisha shughuli za serikali, ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanyika kikao cha kuidhinisha bajeti muhimu iliyohitajika kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wa sekta ya umma kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais wenye ushindani mkali mwezi Disemba mwaka huu.
Mgogoro huu wa kisiasa umesababishwa na uamuzi wa Spika wa bunge la Ghana ambaye alitangaza mwezi Oktoba kuwa viti vinne vya uwakilishi bungeni viko wazi, akisisitiza kuwa wabunge wanne wamevunja katiba kwa kuhama chama.
Mahakama Kuu ya Ghana wiki iliyopita ilibatilisha uamuzi huo ikisisitiza kuwa nafasi za uwakilishi bungeni zilizotajwa kuwa tupu zitawanyima mamia ya maelfu ya raia wa Ghana kuwa wabunge kabla ya uchaguzi wa Disemba 7 mwaka huu.
Kama unavyoona, upande mmoja wa Bunge ni tupu kabisa,” alisema Spika wa Bunge la Ghana, Alban Bagbin, akihutubia katika ukumbi ambao ulikuwa na wabunge wa upinzani pekee kutoka chama cha National Democratic Congress (NDC).