Rais mteule wa Marekani Donald Trump alisema Alhamisi kwamba alizungumza na angalaau viongozi 70 wa dunia tangu ushindi wake wa urais na anadhani atazungumza na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin.
Katika mahojiano na NBC News, Trump alisema alikuwa na “mazungumzo mazuri sana” na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na alizungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.
Akisema kwamba hakuzungumza na Putin, Trump alisema: “Nadhani tutazungumza.”
Matamshi ya Trump yalikuja baada ya Putin kumpongeza kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Jumanne, akisema “Tayari nimesema kwamba tutafanya kazi na mkuu yeyote wa nchi ambaye watu wa Marekani wanamwamini.”
Akizungumza katika kikao cha wajumbe wa Klabu ya Majadiliano ya Kimataifa ya Valdai katika mji wa mapumziko wa Sochi, Putin alisema “alifurahishwa” na tabia ya Trump wakati wa majaribio mawili ya kumuua mwaka huu na kumtaja rais huyo mteule kama “mtu jasiri.”
Rais wa Urusi alidai kuwa Trump “aliwindwa” wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais, jambo ambalo lilimfanya “kuogopa kuchukua hatua.”
Pia alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na Trump.
Kremlin ilisema Alhamisi kwamba haiondoi uwezekano wa mazungumzo kati ya Putin na Trump kabla ya kuapishwa kwake mnamo Januari.
Trump, mgombea wa chama cha Republican, alimshinda mgombea wa chama cha Democratic na Makamu wa Rais Kamala Harris katika kinyang’anyiro cha urais, na kupata angalau kura 295 za Chuo cha Uchaguzi, zaidi ya 270 zinazohitajika.