Mwanamke mmoja huko Thailand akutwa na Sindano ndani ya sehemu zake za siri baada ya miaka 18 kutokana na uzembe wa kitabibu uliofanyika wakati wa kujifungua.
Kulingana na ripoti za Shirika la Pavena Foundation for Children and Women, imeelezwa kuwa Sindano ya kushonea ilianguka ndani ya mwili wake wakati wa kushonwa baada ya kujifungua na haikutolewa, ikimlazimu kuishi na maumivu ya tumbo mara kwa mara kwa miaka mingi.
Mwaka jana, uchunguzi wa X-ray ulibaini kuwa sindano hiyo bado ipo mwilini mwake, ikiwa imekwama ndani ya sehemu zake za siri na Hospitali moja ya Serikali ilimpeleka kwenye Hospitali nyingine kwa ajili ya upasuaji lakini kutokana na Sindano hiyo kusogea ndani ya mwili, upasuaji huo umekuwa ukiahirishwa mara kadhaa.
Kwa sasa, Mwanamke huyo analazimika kwenda Hospitalini mara nne kwa mwezi kwa uangalizi wa Afya, hali inayoongeza mzigo wa kifedha kwa Familia yake licha ya msaada kidogo wa Bima ya Afya, hivyo baada ya kuelemewa kifedha aliomba msaada kutoka kwa Shirika la Pavena Foundation, ambalo limechukua hatua ya kuwasiliana na Ofisi ya usalama wa kijamii kumsaidia katika suala la usafiri.
Hospitali iliyohusika na tukio hili inakabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa jamii, lakini haijatoa kauli yoyote rasmi juu ya kisa hiki hadi sasa.