Polisi wa Paris walisema Jumapili kuwa maafisa 4,000 na wafanyikazi 1,600 wa uwanja watatumwa kwenye mechi inayotarajiwa ya Ufaransa dhidi ya Israel ili kuhakikisha usalama ndani na nje ya uwanja na kwenye usafiri wa umma wiki moja baada ya vurugu dhidi ya mashabiki wa Israeli huko Amsterdam.
Ufaransa na Israel zinacheza mechi ya UEFA Nations League siku ya Alhamisi ambayo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atahudhuria, ikulu ya Elysee ilisema.
Baraza la Usalama la Kitaifa la Israel, katika taarifa yake Jumapili, liliwaonya raia wa ng’ambo kuepuka michezo na matukio ya kitamaduni, haswa mechi ya Paris, na kuwa waangalifu na mashambulio ya vurugu “chini ya kisingizio cha maandamano.”
“Kuna muktadha, mivutano ambayo inafanya mechi hiyo kuwa tukio la hatari sana kwetu,” mkuu wa polisi wa Paris Laurent Nuñez alisema kwenye kituo cha utangazaji cha habari cha Ufaransa BFM TV, akiongeza mamlaka “haitavumilia” vurugu zozote.
Nuñez alisema kuwa maafisa wa polisi 2,500 watatumwa kuzunguka uwanja wa Stade de France, kaskazini mwa mji mkuu wa Ufaransa, pamoja na wengine 1,500 huko Paris na kwa usafiri wa umma.