Takriban watu 14 wamethibitishwa kufariki na wengine wengi kupotea na kudhaniwa kuwa wamekufa baada ya basi kuanguka kwenye mto Indus kaskazini mwa Pakistan, kulingana na mamlaka ya eneo hilo.
Dereva alipoteza udhibiti wa gari hilo alipokuwa akisafiri kwa mwendo wa kasi, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka katika eneo la Gilgit Baltistan, ambako ajali hiyo ilitokea siku ya Jumanne.
Basi hilo lilikuwa limebeba takriban watu 22, washiriki wa maandamano ya harusi, kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Idadi ya waliofariki haijathibitishwa, huku baadhi ya ripoti zikiweka idadi hiyo kuwa juu kama 26.
Vikosi vya uokoaji tayari vimeopoa maiti 13 kutoka mtoni, huku abiria 12 wakiwa hawajulikani waliko na inakisiwa kuwa hawakunusurika katika ajali hiyo kutokana na baridi kali katika eneo hilo, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Pakistani Dawn.
Bibi harusi alinusurika kwenye ajali hiyo na kupelekwa hospitalini, lakini baadaye alifariki dunia, Dawn inaripoti.