Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) imetangaza marufuku ya ndege za Marekani kusafiri kwenye anga ya Haiti kwa muda wa siku 30 baada ya ndege mbili za abiria kushambuliwa kwa risasi. Marufuku hiyo, inayohusu safari katika anga ya chini ya futi 10,000 (sawa na mita 3,048), imewekwa ili kuhakikisha usalama wa abiria na wafanyakazi wa ndege.
Mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu katika anga ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, ambapo ndege za Spirit Airlines na JetBlue Airways zilikumbwa na risasi. Kufuatia tukio hilo, JetBlue ilitangaza kuwa itaongeza muda wa kusitisha safari zake kwenda na kutoka Haiti hadi tarehe 2 Desemba mwaka huu.
Wakati huohuo, Baraza la Rais la Mpito la Haiti limemteua mfanyabiashara na mwanasiasa wa zamani Alix Didier Fils-Aime kuwa Waziri Mkuu mpya, baada ya kumfuta kazi Garry Conille kufuatia mzozo wa kisiasa ulioibuka ndani ya serikali.
Haiti imeendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama licha ya uwepo wa Kikosi cha Usalama cha Kimataifa kinachoongozwa na Kenya na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Taarifa za UN zinaonyesha kuwa watu takriban 4,900 wameuawa nchini humo kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, huku zaidi ya watu 700,000 wakilazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya machafuko yanayohusisha magenge yenye silaha.