Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika, CDC, kimeidhinisha majaribio ya kifaa cha kupima ugonjwa wa mpox kutoka nchini Morocco, taasisi hiyo ikisema hii ni hatua kubwa katika juhudi za kupambana na mlipuko huo barani Afrika.
Kituo cha CDC kimeelezea kuwa kifaa hicho cha kwanza barani Afrika, kina uwezo wa kubaini kwa haraka aina ya virusi vilivyoko katika DNA ya mtu, mate au vimelea vingine vya ugonjwa huu, hatua ambayo taasisi hii inasema inaonesha ufanisi wake.
Mwezi uliopita, shirika la afya duniani WHO liliidhinisha matumizi ya kipimo kingine kutoka kwa kampuni ya Abbot Molecular, chenye uwezo wa kutambua virusi vya mpox kutoka kwa sampuni zilizochukuliwa kutoka kwa vidonda vya binadamu.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, mamlaka barani Afrika zimethibitisha maambukizo ya zaidi ya watu elfu 50, ambapo watu elfu moja wamethibitishwa kufariki, Afrika ya Kati ikiongoza kwa maambukizo na vifo.
Mataifa ya Afrika ya kati yameripoti zaidi ya asilimia 85 ya vifo na maambukizo ya mpox.