Watawala wa kijeshi wa Gabon walisema katiba mpya imeidhinishwa kwa wingi katika kura ya maoni, kulingana na matokeo ya muda yaliyochapishwa Jumapili.
Akizungumza kwenye runinga ya taifa, waziri wa mambo ya ndani alisema asilimia 91.8 ya wapiga kura wamesema “ndiyo” kwa katiba hiyo, na waliojitokeza kupiga kura wanakadiriwa kuwa asilimia 53.5.
Utawala ulio madarakani, unaoongozwa na Rais wa mpito Brice Oligui Nguema, umeahidi kuwa utakuwa hatua muhimu katika kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kidemokrasia, ambao umepangwa kufanyika msimu wa joto wa 2025.
Katika hatua kubwa iliyokaribishwa na Wagabon, maafisa wa kijeshi walichukua mamlaka katika mapinduzi ya Agosti mwaka jana na kumuondoa madarakani Rais Ali Bongo.
Familia yake ilikuwa imedhibiti nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa takriban miaka 60, lakini iliacha uchumi uliodumaa huku thuluthi moja ya watu wakiishi katika umaskini.
Katiba mpya inayopendekezwa imeweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kila mmoja hudumu miaka saba, hakuna waziri mkuu, hakuna ubadilishanaji wa madaraka wa kinasaba, na inatambua Kifaransa kama lugha ya kazi ya Gabon.
Pia inahitaji wagombea urais wawe raia wa Gabon pekee, na angalau mzazi mmoja mzaliwa wa Gabon, na kuwa na mwenzi kutoka Gabon.
Rasimu hiyo, hata hivyo, haimzuii Nguema kugombea urais, na hivyo kuibua wasiwasi kwa baadhi ya watoa maoni kuhusu azma ya junta.
Mahesabu ya mwisho yatatangazwa na Mahakama ya Katiba.