Neymar amefikia makubaliano ya kujiunga tena na Santos mwaka 2025, kulingana na ripoti za kustaajabisha nchini Brazil.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 amekabiliwa na majeraha katika klabu ya Saudi Pro League Al-Hilal na anashughulikia kusitisha mkataba ili kulazimisha kurejea katika klabu yake ya utotoni.
Neymar ameichezea Al-Hilal mara saba pekee tangu uhamisho wake wa Euro milioni 90 kutoka Paris Saint-Germain mwaka 2023 na sasa yuko mbioni kuihama klabu hiyo ya Saudi Arabia, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Brazil Cesar Luis Merlo.
Santos imeripotiwa tayari kufikia makubaliano na supastaa huyo wa zamani wa Barcelona na mazungumzo ya kusitisha mkataba kwa sasa yanaendelea na Al-Hilal.
Neymar alijiunga na Santos akiwa na umri wa miaka 11 na alifanikiwa kupitia safu ya akademi ya kilabu kabla ya kucheza kikosi chake cha kwanza akiwa na umri wa miaka 17 mnamo 2009.
Alicheza mechi 225 za wakubwa katika klabu hiyo, akifunga mabao 136, kabla ya kuondoka na kujiunga na wababe wa La Liga Barcelona kwa €88m Julai 2013. Neymar alitumia miaka minne Camp Nou hadi akawa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka kwa kujiunga na PSG. kwa €222m.