Nchi ya Nigeria, imeanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mpox, ambapo walioanziwa ni wahudumu wa afya na raia wenye kingamwili duni katika hospitali za jiji la Abuja.
Chanjo hii imeanza kutolewa mwezi mmoja kupita tangu serikali ilipopanga zoezi hili kuanza, ambapo mwezi Agosti mwaka huu taifa hilo lilipokea dozi elfu 10 kutoka kwa nchi ya Marekani.
Nigeria, moja ya taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, imerekodi zaidi ya asilimia 90 ya maambukizo ya Mpox huku ikiwa haijarekodi kifo chochote tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Aidha Nigeria ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo mlipuko wa mpox umekuwa ukiripotiwa mara kwa mara, na kuanza kutolewa kwa chanjo hii kunatoa ahueni kwa wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele.
Hadi sasa Afrika ndio imerekodi idadi ya juu ya maambukizi ya Mpox, nchi ya DRC ikiathiriwa zaidi, wakati huu dozi zaidi ya laki 8 zikitolewa kwa mataifa 9 yaliyoathirika zaidi na mpox.