Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya mji wa Njombe,Kuruthum Sadick amewataka wananchi mjini humo kujitokeza katika kampeni za vyama vya siasa zinazoanza November 20 hadi 26 ili kusikiliza sera zitakazowasaidia kuchagua viongozi sahihi.
Kuruthum ametoa kauli wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za halmashauri hiyo ambapo amesema muda wa kampeni ni kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.
Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika kampeni hizo ili waweze kuchagua viongozi sahihi kwa kuwa tayari wagombea wameleta ratiba zao.
“Kwa hiyo mimi nitaomba kwa vyama vyote Chama cha Mapinduzi CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, niombe waweze kufuata utaratibu wa ratiba ambayo walijiwekea ili kuweza kufanya kampeni zao kwa amani,”amesema Kuruthum.
Aidha pia Kuruthum ametoa wito kwa wananchi mjini humo waliojiandikisha kwenye daftari la mkazi kwamba wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakaoongoza katika mitaa, vijiji na vitingoji.
Amesema kwa upande wa makundi maalumu, halmashauri imejipanga kuweka mazingira rafiki ili kila mtu apate nafasi ya kupiga kura bila kikwazo chochote.
“Wananchi wale ambao wanamahitaji maalumu,wamama wenye watoto, wazee na walemavu tumeweza kujipanga kwamba watapewa kipaumbele kwa kuwawekea mazingira rafiki kwa wote,” amesema Kuruthum
Amesema kwa halmashauri hiyo ni vyama vya siasa viwili pekee ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndiyo vilivyosimamisha wagombea.
Nao baadhi ya wananchi mjini Njombe, Akiwemo Mary Mligo amesema wamejiandaa vizuri kupiga kura licha ya wachache kuona kwamba suala hilo halina umuhimu.
“Niwaombe wananchi wenzangu tuanzie kwenye kampeni tukasikilize ili siku ya kupiga kura tukachague viongozi sahihi na tuachane na malalamiko muda sahihi ndio sasa,” amesema Jolam Tweve.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajia kufanyika nchini kote ifikapo Novemba 27 mwaka huu.