Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mnamo Jumanne iliidhinisha uuzaji wa zana na huduma za kijeshi unaoweza kuwa wa dola milioni 100 kwa Ukraine.
“Uuzaji huu unaopendekezwa utasaidia malengo ya sera za kigeni na malengo ya usalama wa kitaifa ya Marekani kwa kuboresha usalama wa nchi mshirika ambayo ni nguvu ya utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi barani Ulaya,” Shirika la Ushirikiano wa Usalama wa Ulinzi lilisema katika taarifa.
Mfuko huo unajumuisha ukarabati wa magari, usaidizi wa kiufundi, mafunzo, machapisho na vifaa na usaidizi, lilisema shirika hilo.
Tangazo hilo limekuja huku kukiwa na ripoti kwamba utawala wa Biden uliidhinisha Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kulenga ndani kabisa ya Urusi. Maafisa wa utawala hawajathibitisha wala kukanusha ripoti hizo.
Hatua hiyo inafuatia ripoti za Korea Kaskazini kutuma wanajeshi kuunga mkono juhudi za vita vya Moscow. Afisa mkuu wa Marekani alisema hatua hiyo pia inalenga kuzuia ushiriki zaidi wa Korea Kaskazini katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, ambavyo vilizinduliwa Februari 2022.
Siku ya Jumanne, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilidai kuwa ilinasa makombora sita ya ATACMS yaliyotolewa na Marekani katika eneo la Bryansk. Ikiwa itathibitishwa, itakuwa alama ya kwanza kwa Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu tangu vita kuanza.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy hangethibitisha au kukanusha kuhusika kwa Kyiv katika mashambulizi ya makombora.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alisasisha fundisho la nyuklia la Moscow Jumanne, kuruhusu uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia kujibu mashambulio ya kawaida ya makombora yanayoungwa mkono na nguvu za nyuklia.