Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Jumanne 19, November 2024 ilifanikiwa kufuzu kucheza AFCON kwa mara ya nne katika historia baada ya kuifunga Guinea goli 1-0 lililofungwa na Simon Msuva dakika ya 61.
Taifa Stars wanafuzu kwa kumaliza nafasi ya pili wakiwa na alama 10, Congo nafasi ya kwanza akiwa na alama 12 wakati Guinea akiwa na alama 9.
Hii ni mara ya nne Taifa Stars kufuzu AFCON itakayopigwa Morocco 2025, mara ya kwanza Tanzania kucheza AFCON 1980 Nigeria, AFCON 2019 Misri, AFCON 2023 Ivory Coast na AFCON 2025 Morocco.
Miongoni mwa waliotoa ujumbe wa pongezi ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi.
‘Hongera sana Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka Arobaini’- Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi.