Waendesha mashtaka mjini New York wameiambia mahakama kuu ya jimbo hilo kwamba watakubali kucheleweshwa kwa hukumu ya rais mteule Donald Trump kwa kukutwa na hatia ya ulaghai wa pesa, lakini wanapinga jaribio lolote la timu ya Trump kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.
Mwezi Mei, Trump alikuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kuhukumiwa kwa uhalifu alipopatikana na hatia ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha pesa za kimyakimya zilizolipwa kwa nyota wa filamu mtu mzima.
Lakini hukumu yake imecheleweshwa mara kwa mara kwa sababu ambazo ni pamoja na athari zinazowezekana kwenye kampeni yake ya uchaguzi wa urais. Mawakili wa utetezi wa Trump wameomba kesi hiyo kutupiliwa mbali.
Siku ya Jumanne, Wakili wa Wilaya Alvin Bragg alituma barua kwa Hakimu wa Mahakama ya Juu ya Jimbo Juan Merchan ili kuwasilisha uamuzi wa upande wa mashtaka.
Barua hiyo ilisema waendesha mashtaka “wanazingatia matakwa na wajibu wa urais,” lakini pia “wanaheshimu sana jukumu la msingi la mahakama” katika mfumo wa kikatiba wa Marekani.
Waendesha mashtaka pia walitaja “haja ya kusawazisha maslahi ya kikatiba yanayoshindana.”