Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameshuhudia uzinduzi wa majaribio ya chombo kikubwa cha anga za juu kinachotengenezwa na SpaceX cha Elon Musk, katika kile ambacho vyombo vya habari vya Marekani vinaeleza kuwa ni ishara ya kukua kwa ukaribu kati ya watu hao wawili.
Siku ya Jumanne, SpaceX ilizindua roketi yake ya Starship kutoka kituo kilichoko kusini mwa jimbo la Texas la Marekani huku Trump na Musk wakihudhuria.
Musk aliunga mkono kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Trump.
Trump alitangaza wiki iliyopita kwamba atamteua Musk kama kiongozi mwenza wa shirika jipya lililopewa jukumu la kukagua na kuzingatia punguzo la matumizi ya serikali.
Baada ya uchaguzi, Musk ameripotiwa kutumia muda mwingi katika makazi ya Trump ya Mar-a-Lago katika jimbo la kusini la Florida.
Mjasiriamali huyo pia inasemekana alikuwepo wakati wa simu kati ya Trump na viongozi wa kigeni na vile vile wakati wa mahojiano na wagombea wa nyadhifa muhimu katika utawala unaoingia.