Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa dhidi ya kuongezeka kwa idadi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini magharibi mwa Urusi.
Zelenskyy aliyasema hayo katika hotuba yake ya mtandaoni kwa Bunge la Ulaya siku ya Jumanne, ikiwa ni siku ya 1,000 tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Wanajeshi wa Korea Kaskazini wametumwa katika eneo la Kursk, magharibi mwa Urusi, ambako vikosi vya Ukraine vinahusika na mashambulizi ya kuvuka mpaka.
Zelenskyy alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin ameleta wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini kwenye mpaka wa Ukraine, na kuonya, “kikosi hiki kinaweza kuongezeka hadi 100,000.” Alitoa wito kwa nchi kuchukua hatua bila kuchelewa, akisema kuwa kadri Putin anavyo muda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya.
Baadaye alikutana na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen na kufanya mkutano wa pamoja wa wanahabari.
Alipoulizwa ikiwa Ukraine imetumia makombora ya masafa marefu ya ATACMS yaliyotolewa na Marekani katika eneo la Urusi, Zelenskyy alikataa kutoa maelezo yoyote.
Rais wa Ukraine alizungumzia tishio la mara kwa mara la Putin la kutumia silaha za nyuklia na kusema siku 1,000 zinatosha kuelewa kwamba kiongozi huyo wa Urusi hataki amani.