Magenge yalianzisha mashambulizi mapya kwenye mji mkuu wa Haiti mapema Jumanne, yakilenga jamii ya watu wa juu huko Port-au-Prince ambapo watu wenye silaha walipambana na wakaazi ambao walipigana bega kwa bega na polisi.
Shambulio hilo dhidi ya Pétionville liliongozwa na kundi la Viv Ansanm, ambalo kiongozi wake, afisa wa zamani wa polisi Jimmy Chérizier, alikuwa ametangaza mpango huo katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii.
Takriban washukiwa 28 wa genge waliuawa na mamia ya silaha kuchukuliwa, kulingana na Lionel Lazarre, naibu msemaji wa Polisi wa Kitaifa wa Haiti.
Haijabainika mara moja ikiwa polisi walikuwa wamejitayarisha kwa shambulio hilo au walijaribu kulinda kwa kuzuia Pétionville ikizingatiwa kwamba Chérizier, ambaye pia anajulikana kama Barbecue, alikuwa ametangaza mipango ya kuishambulia. Lazarre hakurudisha ujumbe kwa maoni.
Mjini Port-au-Prince watu walitembea kuzunguka miili ya waliouawa.
“Kuna wanachama wengi wa magenge ambao waliuawa (na polisi na umma). Wale wanaokimbia wanaenda mafichoni.” Alisema mkazi mmoja wa eneo hilo, ambaye hakutaja jina lake kwa The Associated Press.
Walioshuhudia waliambia The Associated Press kwamba wakaazi walikasirishwa na shambulio lingine la genge kwenye jamii yao. Walisema baadhi ya watu wanaoshukiwa kuwa na bunduki walikatwa vichwa au kukatwa miguu, huku miili ikiwekwa kwenye rundo na kuchomwa moto.
Shambulio la kabla ya alfajiri lilianza wakati malori mawili yaliyokuwa yamewabeba washukiwa wa genge yaliingia Pétionville. Lori moja liliziba lango kuu la kuingilia katika jumuiya hiyo.