Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa idhini ya chanjo aina mpya kutumika dhidi ya Mpox.
Chanjo hiyo imepewa jina la LC16m8 na ni chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya KM Biologics nchini Japan.
Hii ni chanjo ya pili kukubaliwa na WHO kufuatia tamko la Mkurugenzi Mkuu la dharura ya afya ya umma ya kimataifa (PHEIC) tarehe 14 Agosti 2024.
Uamuzi huu unatarajiwa kuwezesha ongezeko na upatikanaji wa chanjo kwa wakati unaofaa katika jamii ambapo milipuko ya Mpox inaongezeka.
“Chanjo ni moja wapo ya zana muhimu zinazosaidia kudhibiti mlipuko kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na Mpox.
Muhimu pia ni uboreshaji wa kupima, kutambua, matibabu na utunzaji wa waliopatikana na Mpox,” Dkt. Yukiko Nakatani, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO anayeshughulikia Upatikanaji wa Dawa na Bidhaa za Afya amesema.
“Chanjo itasaidia huku kukiwa na jitihada za udhibiti wa maambukizi, kushirikisha na kuelimisha jamii zilizoathirika, ” Dkt. Nakatani ameongezea.
Mwaka huu 2024, maambukizi ya Mpox yameripotiwa katika nchi 80, zikiwemo19 barani Afrika, kulingana na data kutoka Oktoba 31, 2024.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi iliyoathiriwa zaidi, ilirekodi idadi kubwa ya maambukizi, zaidi ya wagonjwa 39,000 pamoja na vifo zaidi ya 1000.
Serikali ya Japan imetangaza kutoa dozi milioni 3.05 za chanjo hiyo mpya ya LC16m8, pamoja na sindano maalum za chanjo, kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.