Singapore imeendelea na utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa Mtuhumiwa wa biashara ya Madawa ya kulevya, ikiwa ni mara ya tatu ndani ya wiki moja, Rosman Abdullah, mwenye umri wa miaka 55, alihukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha gramu 57.43 za heroini.
Taasisi ya kudhibiti Madawa ya kulevya nchini humo ilithibitisha kuwa Rosman alipata haki kamili za kisheria na alikuwa na uwakilishi wa kisheria katika kila hatua ya mchakato wa kesi yake aidha Serikali ya Singapore imeendelea kutetea adhabu ya kifo ikisema inalenga kuzuia uhalifu mkubwa kama biashara ya Madawa ya kulevya ambayo huleta madhara makubwa kwa Jamii.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na Mashirika ya haki za Binadamu kama Amnesty International yalitoa wito wa kuahirishwa kwa hukumu hiyo ambapo Umoja wa Mataifa ulieleza wasiwasi wake juu ya uwezo wa Rosman kushiriki kikamilifu katika kesi yake kutokana na changamoto za ulemavu wa kiakili alizokuwa nazo.
Rosman alinyongwa katika Gereza la Changi, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kunyongwa kwa Raia wa Malaysia mwenye umri wa miaka 39 na Msingapore mwingine wa miaka 53 kwa kosa hilo, inaelezwa tangu kuanza tena utekelezaji wa adhabu ya kifo mwaka 2022 baada ya kusimama kwa muda kutokana na janga la COVID-19, Singapore imefanya jumla ya hukumu 24 za kunyongwa, nane kati ya hizo zikiwa mwaka huu pekee.
Licha ya kushutumiwa kimataifa, Serikali ya Singapore imeendelea kusisitiza kuwa adhabu ya kifo ni muhimu katika kupambana na uhalifu wa Madawa ya kulevya, ikidai kuwa Wananchi wengi wanaunga mkono sheria hiyo.