Rais wa Urusi Vladimir Putin ametia saini sheria ya kutoa msamaha wa madeni kwa wale wanaojiunga na jeshi. Hatua hiyo iliyochukuliwa siku ya Jumamosi inaonekana kuwa ni hatua ya kuajiri wanajeshi zaidi kupigana katika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Sheria inatoa msamaha wa deni katika malimbikizo ya hadi rubles milioni 10, au karibu dola 96,000, kwa waajiri wapya ikiwa watasaini mkataba wa mwaka mmoja au zaidi mnamo Desemba 1 au baadaye. Hatua hiyo pia inatumika kwa wenzi wao.
Utawala wa Putin umekuwa ukijaribu kuajiri wanajeshi wa kandarasi badala ya kuongeza uhamasishaji wa wanajeshi, ambao umekabiliwa na kutoridhika kwa umma.
Malipo ya juu kwa askari wa kandarasi na msamaha kwa wafungwa waliopatikana na hatia wanaojiandikisha jeshini vimetolewa.
Urusi pia inaonekana kuwaajiri raia wa kigeni ili kuimarisha vikosi vyake vya kupigana nchini Ukraine.
Gazeti la Financial Times liliripoti Jumapili kwamba Urusi imetuma mamia ya mamluki wa Yemen katika mstari wa mbele nchini Ukraine.
Ripoti hiyo inasema watu hao walipewa kazi, mishahara minono na hata uraia wa Urusi, lakini walilazimishwa kujiunga na jeshi baada ya kuwasili Urusi.