Iran ilisema Jumapili kuwa itafanya mazungumzo ya nyuklia katika siku zijazo na nchi tatu za Ulaya ambazo zilianzisha azimio la kulaani dhidi yake lililopitishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Esmaeil Baghaei amesema mkutano wa manaibu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza utafanyika siku ya Ijumaa, bila kutaja mahali patakapofanyika.
“Masuala na mada mbalimbali za kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na masuala ya Palestina na Lebanon, pamoja na suala la nyuklia, zitajadiliwa,” msemaji huyo alisema katika taarifa ya wizara ya mambo ya nje.
Baghaei aliutaja mkutano ujao kuwa ni mwendelezo wa mazungumzo yaliyofanyika na nchi hizo mwezi Septemba kando ya kikao cha mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Siku ya Alhamisi, bodi ya magavana wa mataifa 35 ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki wa Umoja wa Mataifa (IAEA) ilipitisha azimio la kulaani Iran kwa kile ilichokiita ukosefu wa ushirikiano.
Hatua hiyo imekuja huku mvutano ukiongezeka kuhusu mpango wa atomiki wa Iran, ambao wakosoaji wanahofia kuwa unalenga kutengeneza silaha za nyuklia — jambo ambalo Tehran imekanusha mara kwa mara.
Kujibu azimio hilo, Iran ilitangaza kuwa inazindua “msururu wa vituo vipya na vya hali ya juu”.