Vikosi vya Israel vinasema kuwa kundi la Waislamu wa Dhehebu la Shia lenye makao yake nchini Lebanon, Hezbollah lilirusha takribani roketi 160 dhidi ya Israel siku ya Jumapili huku kukiwa na mapigano makali kati ya Israel na kundi hilo.
Vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa shambulio hilo la roketi lilijeruhi watu kadhaa na kusababisha uharibifu wa nyumba.
Jana Jumapili, jeshi la Israel liliendelea na mashambulizi yake ya anga kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Mamlaka za afya za Lebanon zinasema watu wasiopungua 29 waliuawa katika shambulio la anga la Israel huko Beirut juzi Jumamosi na kujeruhi wengine 67.
Mazungumzo kuhusu kusitisha mapigano pia yameendelea.
Jana Jumapili, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alitembelea Lebanon na kukutana na spika wa bunge la Lebanon Nabih Berri.
Borrell alisema baada ya mkutano huo, “Lazima tuishinikize serikali ya Israel na kudumisha shinikizo kwa Hezbollah kukubali pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano.”