Jimbo la New York limefuta rasmi sheria ya zamani iliyokuwa ikifanya kuchepuka kuwa kosa la jinai ambapo katika Sheria hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1907, iliwahi kumfunga Mtu kwa miezi mitatu kwa kosa la kudanganya mwenza wake, lakini haikutumika mara kwa mara.
Gavana Kathy Hochul alisaini mswada wa kufuta sheria hiyo na kusema kuwa masuala ya Ndoa yanapaswa kushughulikiwa kati ya wahusika wenyewe, si kupitia mfumo wa sheria huku akisisitiza kuwa sheria hiyo haikuwa na maana tena katika nyakati za sasa.
Sheria hiyo ilianzishwa ili kufanya talaka kuwa ngumu zaidi wakati kuchepuka kulionekana njia pekee ya kuthibitisha hitaji la talaka hata hivyo, mashitaka chini ya sheria hii yalikuwa machache sana na kesi za hatia zilikuwa nadra.
Tangu miaka ya 1970 ni Watu wachache waliowahi kushtakiwa kwa sheria hiyo na ni wachache waliopatikana na hatia huku mara ya mwisho kutumika kwa sheria hii ilikuwa mwaka 2010 lakini shtaka hilo liliondolewa kupitia makubaliano ya Mahakama.
Kufutwa kwa sheria hii sasa kunahitimisha safari ya kuondoa kanuni ya zamani ambayo haikuwa na umuhimu tena katika jamii ya kisasa.