Msanii wa muziki Grimes, jina lake halisi Claire Boucher, ameeleza changamoto alizokutana nazo katika kesi ya malezi dhidi ya aliyekuwa mwenzi wake, Elon Musk.
Kupitia mtandao wa X, Grimes alisema alitumia mwaka mzima kupigania haki zake kama mama, akimwelezea Musk kama “mtu asiyeweza kutambulika”.
Grimes alieleza kuwa machapisho yake ya mitandaoni yalitumiwa dhidi yake katika kesi hiyo, ambayo ilihusisha watoto wao watatu: X AE A-12 mwenye miaka 4, Exa mwenye miaka 2, na Tau pia mwenye miaka 2. Ripoti zinasema kuwa mgogoro huo sasa umehitimishwa.
Akiendelea, Grimes alisema changamoto hizo zilimfanya akose muda wa kumuona mmoja wa watoto wake kwa miezi mitano, huku akibeba mzigo mkubwa wa kifedha uliotishia kumfilisi.
Hata hivyo, alisema uzoefu huo ulimfundisha mambo mengi na kuimarisha ubunifu wake.
Grimes na Musk walitangaza kutengana Machi 2022 baada ya kuwa pamoja kwa miaka minne. Kesi ya malezi ilianza Septemba mwaka huo na kufungwa rasmi Desemba, huku maamuzi yakiwa ya siri. Katika chapisho lililofutwa, Grimes alidokeza kuwa anashirikiana malezi na Musk, akisema anapata muda wa kuwa na watoto wake kila wiki moja kwa zamu.
Licha ya changamoto hizo, Grimes alisema sasa anajisikia kuwa bora zaidi, huku akibainisha kuwa watoto wake wamempa mtazamo mpya wa maisha na kumsaidia kukuza ubunifu wake.